Saturday, April 1, 2023

Jumapili ya matawi

 𝐈𝐅𝐀𝐇𝐀𝐌𝐔 𝐉𝐔𝐌𝐀𝐏𝐈𝐋𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐓𝐀𝐖𝐈.


Jumapili ya matawi ni jumapili moja kabla ya sherehe ya 𝐏𝐚𝐬𝐚𝐤𝐚 ambayo kwa mujibu wa Injili, Kanisa Katoliki huanza 𝐰𝐢𝐤𝐢 𝐭𝐚𝐤𝐚𝐭𝐢𝐟𝐮 kwa lengo la kukumbuka mateso, kifo na ufufuko wa 𝐁𝐰𝐚𝐧𝐚 wetu 𝐘𝐞𝐬𝐮 𝐊𝐫𝐢𝐬𝐭𝐨.


Pia ndiyo siku maalumu ambayo Wakristo wengi hukumbuka na kusherekea siku ile 𝐘𝐞𝐬𝐮 alipoingia Yerusalemu kwa mara ya mwisho kama 𝐌𝐰𝐨𝐤𝐨𝐳𝐢 na 𝐌𝐟𝐚𝐥𝐦𝐞 wao.


Inasemekana kuwa, siku hiyo 𝐘𝐞𝐬𝐮 alipokuwa anaingia Yerusalemu alipanda punda huku umati mkubwa wa watu hasa vijana wakimfuata kwa furaha, wengine walishika matawi na kutandaza nguo zao chini ili kumpa 𝐘𝐞𝐬𝐮 heshima ya Kifalme na kuimba:


"𝐇𝐨𝐬𝐚𝐧𝐚 𝐌𝐰𝐚𝐧𝐚 𝐰𝐚 𝐃𝐚𝐮𝐝𝐢, 𝐧𝐝𝐢𝐲𝐞 𝐌𝐛𝐚𝐫𝐢𝐤𝐢𝐰𝐚, 𝐲𝐞𝐲𝐞 𝐚𝐣𝐚𝐲𝐞 𝐤𝐰𝐚 𝐣𝐢𝐧𝐚 𝐥𝐚 𝐁𝐰𝐚𝐧𝐚, 𝐡𝐨𝐬𝐚𝐧𝐚 𝐣𝐮𝐮 𝐌𝐛𝐢𝐧𝐠𝐮𝐧𝐢". (𝐌𝐚𝐭𝐡𝐚𝐲𝐨 21:1-11)


Neno la Mungu linatuambia kwamba, tukio hilo la kupunga matawi na mengine kuyatandaza chini ili 𝐘𝐞𝐬𝐮 apite juu yake, basi matawi hayo yaliwakilisha mema na alama kubwa ya ushindi juu ya kifo alichokishinda Yesu baada ya siku tatu alipofufuka kaburini. (1𝐖𝐚𝐤𝐨𝐫𝐢𝐧𝐭𝐡𝐨 15:55)


Lakini pia kitendo cha 𝐘𝐞𝐬𝐮 kupanda punda, ilikuwa ni kutimiza ule unabii uliotolewa tangu kale juu ya ufalme wake, maana nyakati zile Wafalme wa Kisraeli walipokuwa wakilakiwa na watu huwa wanapanda punda, huku wakiimbia nyimbo za kishujaa.


Kibiblia "𝐏𝐮𝐧𝐝𝐚" huwakilisha amani, kwahiyo wale waliomlaki 𝐘𝐞𝐬𝐮, walionesha kujawa na amani, kwa kuwa walimuona 𝐘𝐞𝐬𝐮 kama 𝐌𝐟𝐚𝐥𝐦𝐞 wao atakayeleta amani ndani ya taifa la Israeli.  (𝐙𝐞𝐤𝐚𝐫𝐢𝐚 9:9)


Kadhalika hata neno "𝐇𝐨𝐬𝐚𝐧𝐚" Kibiblia lilimaanisha "𝐎𝐤𝐨𝐚 𝐬𝐚𝐬𝐚",  hivyo Waisraeli walimwiimbia 𝐘𝐞𝐬𝐮 wimbo huo wakiamini kwamba, muda si mrefu yule 𝐌𝐚𝐬𝐢𝐡𝐚 waliomgojea ataenda kuwaokoa dhidi ya ukatili, manyanyaso na dhuluma ya dola ya kirumi iliyokuwa inatawala nchi yao.


Ingawa Biblia inafunua wazi kuwa, japo Waisraeli walimuona 𝐘𝐞𝐬𝐮 kama 𝐌𝐟𝐚𝐥𝐦𝐞 wao kwenye mambo ya siasa, kumbe 𝐘𝐞𝐬𝐮 hakuja ulimwenguni kwa ajili hiyo, bali alikuja ili kutuokoa kutoka kwenye dhambi ya mauti na kifo, na hiyo ndiyo ilikuwa ajenda kuu ya utume wake alioufanya hapa duniani miaka 2000 iliyopita. (𝐘𝐨𝐡𝐚𝐧𝐞 12:12-15, 𝐙𝐚𝐛𝐮𝐫𝐢 118:25-28 na 𝐖𝐚𝐫𝐮𝐦𝐢 10:9)


Pia hata 𝐘𝐞𝐬𝐮 alipokuwa anaukaribia mji, Biblia inatuambia kwamba aliulilia sana kwa machozi licha ya kushangiliwa kwa furaha na watu waliomzunguka. Maana alitambua kuwa, muda si mrefu wale wanaomshangilia ndio watakaomsaliti na kumuua kwa kifo cha aibu na maumivu makali pale Msalabani Kalvari. (𝐋𝐮𝐤𝐚 19:41-42)


Hivyo nihitimishe kwa kusema kwamba, jumapili hii ya matawi itukumbushe kufahamu kuwa 𝐘𝐞𝐬𝐮 𝐊𝐫𝐢𝐬𝐭𝐨 ndiye 𝐌𝐤𝐮𝐮 kuliko mtu yeyote yule duniani, na hii ndiyo sababu kuu ya kusherekea juma hili, kwani kupitia sadaka ya kifo chake pale Msalabani, sote tuliwekwa huru kutoka mauti na kuingizwa kwenye furaha ya uzima wa milele.


Basi ndugu zangu 𝐘𝐞𝐬𝐮 tunayemshangilia leo, tukamshangilie siku zote katika maisha yetu kwa kutenda mema na kuacha maovu wala tusimsaliti kama vile Waisraeli walivyofanya, bali tuwe waaminifu kwa Mungu na jirani zetu, maana usaliti sio mzuri, inaweza kuondoa amani na kuleta machafuko pamoja na mauaji kwa wale wanaotuamini, hivyo tujifunze kupitia tukio hili la matawi ili tuishi vizuri na wenzetu.


𝐀𝐬𝐚𝐧𝐭𝐞 𝐧𝐚 𝐌𝐮𝐧𝐠𝐮 𝐚𝐰𝐚𝐛𝐚𝐫𝐢𝐤𝐢...

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home